HAKUNA UTHIBITISHO WA UWEPO WA NZIGE WA JANGWANI NCHINI- WAZIRI WA KILIMO MHE. HASUNGA

HAKUNA UTHIBITISHO WA UWEPO WA NZIGE WA JANGWANI NCHINI- WAZIRI WA KILIMO MHE. HASUNGA

HAKUNA UTHIBITISHO WA UWEPO NZIGE WA JANGWANI NCHINI-WAZIRI HASUNGA- Dodoma. Serikali imewatoa hofu wakulima nchini kuwa hakuna taarifa za uthibitisho wa uwepo wadudu hatari aina ya Nzige wa Jangwani walioripotiwa katika nchi za jirani. Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo (29.01.2020) wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma na kusema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kufuatiliaji viashiria vya uwepo wa Nzige wa Jangwani (Locust Desert). “Hadi sasa hakuna uthibitisho wa kitaalam kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani nchini Tanzania” alisisitiza Waziri Hasunga Alibainisha wazi kuwa Serikali imejipanga kuwadhibiti nzige hao endapo wataingia nchini na tayari ina lita 7,000 za viuatilifu kwa ajili ya tahadhari ya kukabiliana na tishio hilo na ununuzi wa viuatilifu vingine zaidi unaendelea kufanyika. Alisema Wizara yake inaendelea kuchukua tahadhali kuhakikisha visumbufu vya mazao ya kilimo kama Nzige Wekundu, Ndege waharibifu wa nafaka aina ya Kwelea kwelea, panya na Kiwavijeshi Vamizi zinaripotiwa na kudhibitiwa kwa haraka. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo tishio la Nzige wa Jangwani limeripotiwa katika nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na Kenya hivyo kuwepo uwezakano wa Tanzania kuvamiwa na Nzige hao. “Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoweza kuathirika na aina mbili za Nzige yaani Nzige Wekundu na Nzige wa Jangwani hivyo tumejipanga kuwadhibiti wakitokea” alisema Waziri wa Kilimo. Waziri wa Kilimo amewataka wataalam wa kilimo kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasimamia Maafisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao ili kuhakikisha kwamba wanawatembelea wakulima mashambani na kubaini endapo kuna viashiria vya uwepo wa Nzige. Serikali itaendelea kuhakikisha visumbufu vya mimea na mazao vinadhibitiwa ili wakulima wavune mazao yao kwa wingi na nchi kuendelea kuwa na uhakika wa chakula. Mwisho