Rais Magufuli Azindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II)

Rais Magufuli Azindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Juni, 2018 amezindua Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme, Phase Two – ASDP II). Mpango huo wa miaka mitano utatekelezwa hadi mwaka 2023 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 13.8 ambapo Serikali na washirika wa maendeleo watatoa asilimia 40 ya fedha hizo, na sekta binafsi itatoa asilimia 60.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, wadau wa sekta binafsi, viongozi wa dini na viongozi wa siasa.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi na wataalamu wa Serikali pamoja wadau wengine ikiwemo sekta binafsi, kusimamia vizuri utekelezaji wa mpango huo ambao lengo lake kuu ni kuleta mageuzi katika sekta ndogo za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi badala ya kujikimu pekee, kuongeza mapato ya wakulima, uhakika wa usalama wa chakula na lishe na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa Serikali itashirikiana nao kwa karibu katika utekelezaji wa mpango huu, lakini ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa benki ya maendeleo ya kilimo ambayo amesema licha ya kuwezeshwa na Serikali mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, imekuwa haiwakopeshi wakulima.

“Naomba niwe mkweli, bado sijaridhika na utendaji kazi wa benki hii, benki ipo pale kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, Serikali inakopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, lakini yenyewe inachukua hizo hela na kwenda kuzikopesha benki zingine.

“Kwa hiyo tumekopa pesa kutoka AfDB Shilingi Bilioni 207, mtaji umewekwa na Serikali Shilingi Bilioni 60 tangu mwaka 2014, lakini hakuna fedha iliyokwenda kwa mkulima, na wakati mwingine benki hii inapotaka kukopesha huwatafuta matajiri wakubwa ambao baadhi yao wameshindwa kulipa mikopo yao kwenye benki zingine, sasa nikisema siridhiki na utendaji wa benki hii mtanikatalia ndugu zangu?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Serikali kutoa taarifa juu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) ambao mwaka 2016 ulipatiwa Shilingi Bilioni 150 za mkopo kutoka Benki ya Dunia na mradi wa kuunganisha matrekta uliopatiwa mkopo wa takribani Shilingi Bilioni 248.