Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imeeleza kuwa imekusudia kuhakikisha kuwa mbegu bora za kilimo zinazalishwa nchini ili kuondokana na wimbi la uagizaji wa mbegu nje ya nchi.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo (tarehe 22 Disemba 2019) alipotembelea kampuni ya Namburi inayojihusisha na uzalishaji wa mbegu za vizazi za mahindi, mtama na mpunga iliyopo katika eneo la Vwawa wilayani Mbozi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe hivi karibuni.
Amesema kuwa Tanzania ina uhitaji wa mbegu kiasi cha Tani 186,000 za mazao mbalimbali huku uzalishaji wa ndani ikiwa ni pamoja na uagizaji wa mbegu nje ya nchi ukiwa bado mdogo kwani haujafika hata Tani 50,000.
“Tanzania ina maeneo makubwa na bora kwa uzalishaji hivyo ni lazima kuzalisha mbegu za kutosha nchini kwa kutumia umwagiliaji na kuachana na utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi” alisema Waziri Hasunga
Katika ziara hiyo Waziri Hasunga alikagua skimu ya umwagiliaji ya kijiji cha Mbulu wilaya ya Mbozi na kuwaeleza wakulima kuwa nchi yetu itafanikiwa kuongeza uzalishaji mbegu endapo tutawekeza kwenye umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua.
“Kilimo cha kutegemea mvua ni hatari kwani hakina uhakika wa upatikanaji wa chakula cha kutosha kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi” alisema Hasunga.
Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo huyo amewaagiza maafisa ugani nchini kote kuzuru katika maeneo ya wakulima ili kutoa elimu sahihi za kilimo, matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na matumizi sahihi ya zana za kilimo.
Waziri Hasunga amesema wizara inatekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) yenye jukumu la kuimarisha masoko na kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha wakulima wanatumia kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kupata elimu bora na juu ya matumizi ya teknolojia.
Waziri Hasunga amesema kuwa Programu ya ASDP II inasisitiza matumizi bora ya maji na ardhi, hivyo sekta ya kilimo ni muhimili wa matumizi bora ya maji kupitia skimu za umwagiliaji ambapo uzalishaji wa mbegu bora utapatikana.
Tanzania ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lenye jumla ya hekta milioni 29.4 ambapo kati ya hizo,hekta milioni 2.3 zina uwezo mkubwa wa kuendelezwa, hekta milioni4.8 zina uwezo wa kati ;na hekta milioni 22.3 zina uwezo mdogo wa kuendelezwa.