Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme phase Two-ASDP II) ilizinduliwa tarehe 4 Juni 2018na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli. Programu itatekelezwa kwa muda wa miaka kumi kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2027/2028 katika awamu mbili ambazo zimegawanyika katika vipindi viwili vya miaka mitano (5) kwa kila awamu. Awamu ya kwanza ya utekelezaji imeanza mwaka 2017/18 na kufikia mwisho mwaka 2022/23 na awamu ya pili ya utekelezaji itaanza mwaka 2023/24 na kufikia mwisho mwaka 2027/28. ASDP II ni mwendelezo wa utekelezaji wa Awamu yaKwanza ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo iliyotekelezwa kwamiaka saba kuanzia mwaka 2006/2007 hadi 2013/2014. Hivyo maandalizi ya utekelezaji wa ASDP II yamezingatia mahitaji ya sasa ya nchi na ajendaya kufikia uchumi wa kati na pia uzoefu uliotokana na utekelezaji wa awamu ya kwanza ya programu.
ASDP II inalenga kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza kipato cha wakulima wadogo na wa kati ili kuboresha maisha yao, kuongeza uhakika wa usalama wa chakula na lishe na piakuongeza Pato la Taifa . Mkakati wa ASDP II ni kuwabadilisha wakulima wadogo na wakati kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kibiashara.